Lugha

Aya za Qur’ani kwa wasomaji Wakristo

Kwa jina la Mungu wa kweli aliye Mmoja tu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

Sema: 'Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lililo sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote. Wala tusifanyane waungu sisi kwa sisi badala ya Mwenyezi Mungu.' Na wakigeuka, basi semeni: Shuhudieni ya kwamba sisi kwa hakika ni Waislamu.

Hakika, Dini kwa Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na hawakuhitilafiana wale waliopewa Kitabu isipokuwa baada ya kujiwa na elimu, kwa sababu ya uhasidi uliokuwa baina yao. Na mwenye kuzikufuru Ishara za Mwenyezi Mungu, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu. Na wakikuhoji, basi sema: Mimi nimeusalimisha uso wangu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na vile vile walionifuata. Na waambie wale waliopewa Kitabu na wale wasiojua kusoma: "Je, mmesilimu?" Wakisilimu, basi hakika wameongoka. Na wakikengeuka, basi juu yako ni kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona vyema waja wake.

Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu bila ya haki. Wala msifuate matamanio ya kaumu waliokwishapotea tangu zamani, na wakawapoteza wengi, na wenyewe wakapotea njia iliyo sawa.

Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msiseme juu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa haki tu. Hakika, Masihi Isa mwana wa Maryam ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilomfikishia Maryam, na ni roho iliyotoka kwake. Basi Muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Wala msiseme: 'Utatu.' Komekeni! Itakuwa heri kwenu. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ametakasika Yeye na kuwa na mwana. Ni vyake Yeye vyote vilivyo katika mbingu na vilivyo katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mtegemewa.

Haikumfailia mtu yeyote kwamba Mwenyezi Mungu ampe Kitabu na hekima na Unabii, kisha awaambie watu: 'Kuweni wa kuniabudu mimi badala ya Mwenyezi Mungu.' Bali atawaambia: 'Kuweni wenye kumuabudu Mola Mlezi wa viumbe vyote, kwa kuwa nyinyi mnafundisha Kitabu na kwa kuwa mnakisoma.' Wala hatawaamrisha kwamba muwafanye Malaika na Manabii kuwa ni miungu. Je, atawaamrisha ukafiri baada ya nyinyi kuwa Waislamu?

Na hakika, miongoni mwa Watu wa Kitabu kuna wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu na yaliyoteremshwa kwenu na yaliyoteremshwa kwao, wakimnyenyekea Mwenyezi Mungu. Hawanunui kwa Aya za Mwenyezi Mungu thamani ndogo. Hao wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu.[1]

Na wanaposikia yale yaliyoteremshwa kwa Mtume, utayaona macho yao yanamiminika machozi kwa sababu ya haki waliyoitambua. Wanasema: Mola wetu Mlezi! Tumeamini. Basi tuandike pamoja na wanaoshuhudia. Na kwa nini tusimwamini Mwenyezi Mungu na haki iliyotujia, na hali tunatumai Mola wetu Mlezi atuingize pamoja na kaumu ya walio wema? Basi Mwenyezi Mungu akawalipa kwa yale waliyoyasema, Mabustani yapitayo mito kwa chini yake, wadumu humo. Na hayo ndiyo malipo ya wafanyao wema. Na wale waliokufuru na wakazikadhibisha ishara zetu, hao ndio watu wa Jahiim.

Bonyeza hapa kuendelea

Makala kuhusu Uislamu

Maelezo ya tafsiri

3:199 [1] Imani yao ilipokuwa ya ujumla (bila ya kutofautisha baina ya Manabii na Vitabu), na ya uhakika, ikawa ni ya manufaa. Kwa hivyo, ikawafanya kumnyenyekea Mwenyezi Mungu. Na katika ukamilifu wa kumnyenyekea kwao Mwenyezi Mungu ni kwamba, "hawanunui kwa Aya za Mwenyezi Mungu thamani ndogo." Kwa hivyo, hawaitangulizi dunia mbele ya dini kama walivyofanya watu wa upotovu, ambao wanaficha yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu na kununua kwayo thamani ndogo. Na wakajua kwamba katika hasara kubwa zaidi ni kutosheka na kilicho duni badala ya dini.